Tuesday, October 29, 2013

UKAKASI KTK MIEZI 18 YA UTENDAJI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA




Novemba 1 mwaka, huu Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitimiza miezi 18 tangu ianze kazi za kuratibu mchakato wa Katiba. Ni wakati ambao ilitarajiwa iwe imewasilisha rasimu ya pili ya Katiba, kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa serikali ya Zanzibar.

Hatua hiyo haijatekelezwa, kutokana na ombi la tume hiyo kuongezewa mwezi mmoja, ili kukamilisha kazi hiyo na kuikabidhi kwa mamlaka husika. Hata hivyo, kumeibuka taarifa kwamba wajumbe wengi wa tume hiyo, wapo hatarini kiafya.


Hatari hiyo inaelezwa kutokana na ufinyu wa muda, ambao umepangwa bila kutilia maanani taratibu za kiafya, ikizingatiwa kuwa wengi wa wajumbe wa tume hiyo ni wenye umri usiopungua miaka 60
Kufuatia tetesi hizo, tukafuatilia ratiba ya utendaji wa tume hiyo, katika hatua inayotekelezwa; 
Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba

Kuboresha rasimu ya Katiba, kwa kutumia maoni yaliyotolewa na mabaraza ya Katiba ya wilaya zote nchini, taasisi, asasi na jumuiya zenye mtazamo unaofanana zisizopungua 600

Naibu Katibu wa tume, Casmir Kyuki anasema, 
“Tunafanya kazi siku zote za kazi including (ikiwamo) Jumapili, vikao vinaanza rasmi Saa 3: asubuhi mpaka Saa 7: tunapumzika kisha Saa 9: tunaendele; kumaliza inategemea na kundi limemaliza saa ngapi kwasababu wamegawanywa katika makundi; kwa mfano jana kuna walioondoka Saa 5: usiku.”

Daktari wa Afya ya binadamu, Dk. Joseph Masanja anasema mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 60 anapolazimika kufanya kazi ya kutumia zaidi akili, inatakiwa pamoja na mambo mengine, muda wa kufanya kazi uwe kati ya Saa Nne hadi Sita kwa siku; wenye umri chini ya huo wanaweza kufanya kazi kati ya Saa Sita hadi Nane kwa siku.

“Mazingira wanayofanyia kazi yanatakiwa yasiwe na viyoyozi (AC), kama ni lazima basi umakini unahitajika katika kuvitumia; Kinyume chake wataugua vichomi, (Pneumonia),” Dk. Dk.Masanja alisema

Dk.Masanja anasema kwa umri huo, mwili wa binadamu unakuwa katika hatari ya kushambuliwa na magonjwa, wengi wanakuwa  wanaugua Kisukari na Shinikizo la damu; kutozingatia umri, aina ya kazi na mazingira ni kuchochea magonjwa zaidi kwa muhusika.

“…, miili haishughulishwi vya kutosha, wafanye mazoezi sana ili mafuta yasijikusanye na kuganda kwenye mishipa, hali inayoweza kusababisha shinikizo la damu na hata kupooza mwili,” alieleza Dk. Masanja

Wajumbe hao wanaelezwa pia kuwa katika hatari ya kuugua ugonjwa utokanao na uchovu (fatique). Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na mtu kuwa na hasira za haraka, kukosa hamu ya kulala, kutolala usingizi vya kutosha au kukosa kabisa usingizi na mwili kuchoka.

Hata hivyo, mjumbe wa tume hiyo, Joseph Butiku alisema, “Fatigue ipo kila mahala, hata wewe unayetafuta na kuandika habari unaweza kuugua, hapa tunafanya kazi zetu kama kawaida tu, watu wengine wanapenda kukuza mambo.”

Jumamosi iliyopita, tulifika nyumbani kwa Mjumbe mwingine wa tume hiyo, John Nkolo, kumjulia hali baada ya kuugua akiwa kazini wilayani Sengerema, wakati tume ikiratibu maoni ya mabaraza ya Katiba ya wilaya.
Naibu Waziri wa Afya nchini, Dk. Seif Rashid

Baadaye uchunguzi wa madaktari ulibaini kuwa Nkolo, alipatwa na ugonjwa wa kupooza upande wa kulia; usoni na kwa maelezo ya mke wake, Joyce John, Daktari alisema ni bahati nzuri kwamba ubongo wake haukuathiriwa na ugonjwa huo. 

Sasa anafanya mazoezi ya viungo, ingawa hajaweza kuzungumza vizuri
 
Wiki mbili zilizopita, ziiliibuka tetesi kuwa afya ya Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba siyo nzuri na kwamba alikuwa nje ya nchi, kutibiwa. 

Tulimpigia simu yake ya kiganjani, ikapokewa na mwanamke aliyejitambulisha kuwa ni mke wake, akasema Jaji alikuwa nje ya nchi lakini hakuwa tayari kutaja nchi gani.

Mahojiano kati ya Mwandishi na Makamu mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Augustino Ramadhan, juu ya tetesi hizo yalifanyika hivi;
Mwandishi: Tuna taarifa kwamba afya ya mwenyekiti siyo nzuri, yupo nchini India akifanyiwa uchunguzi tunaomba kufahamu anavyoendelea.

Jaji Ramadhan: Eeeeh, mimi nipo Iringa, ila ni kweli mwenyekiti yupo India for checkup, (kuchunguzwa afya)ebu wasiliana na Katibu anaweza kukupa ufafanuzi zaidi.

Katibu wa tume, Assa Rashid hakupokea simu yake ya kiganjani kila alipopigiwa hali iliyosababisha atafutwe makamu wake,Casmir Kyuki;

“Nani amewaambia mwenyekiti yupo India?, Aliyewapa hizo taarifa kwanini asiwathibitishie? Kwani wewe ukienda Agha Khan kuonana na daktari, utakuwa mgonjwa?” alihoji Kyuki na kuendelea

“Yule (Jaji Warioba) kwa wadhifa wake (waziri mkuu mstaafu)anahudumiwa na serikali kuu na kwa umri wake siyo ajabu kuwa na utaratibu wa kufanyiwa checkup kila baada ya muda fulani, siyo mpaka augue; kwahiyo ikiwa yupo India labda ameenda kwa ajili hiyo.”

Mjumbe mwingine wa tume hiyo, Dk. Edimund Mvungi anasema, “Sioni kwanini mtu afiche ukweli uliyo wazi, tunafanya kazi kwa kasi ya ajabu; binafsi huwa naingia ofisini saa 12:45 kutoka inategemea muda wa kumaliza vikao…, wakati naingia tume nilikuwa na tatizo la Kisukari, Pressure imenianza nikiwa humu,” anaeleza Mvungi

Utafiti umebaini kuwa kwa muda wote huo, sera ya tume hiyo haina bima ya afya ya watendaji wake, mtu anapougua anatakiwa kujihudumia kisha kupeleka madai ili alipwe. 

Hoja ya msingi hapa ni; Watanzania watapata Katiba itakayowaletea matokeo wanayoyatarajia? Tukutane Juma lijalo, ambapo tutakuletea athari za hali hii katika ufanisi wa kazi.


Friday, October 25, 2013

PPF IMETUMIA 3 BIL KUSOMESHA YATIMA WA WANACHAMA WAKE



Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio, akizungumza kwenye mkutano na Kamati ya Bunge ya masuala ya UKIMWI
Mkurugenzi wa Mfuko wa Akiba wa PPF, William Erio akizungumza na Kamati ya Kudumu ya Bunge, ya masuala ya UKIMWI na dawa za kulevya leo, katika makao makuu ya mfuko huo jijini Dar es Salaam.

Mfuko huo kwa miaka 10 umeelezwa kutumia Sh. Bilioni 3 kusomesha watoto waliofiwa na wazazi wao, ambao walikuwa wananchama wake na tangu Januari mpaka Juni mwaka huu, Sh milioni 615 zimetumika kusomesha yatima 1,151; kuanzia chekechea hadi kidato cha nne.
Mwakani, mfuko huo utaongeza ufadhili huo kwa kusomesha watoto wa aina hiyo mpaka kidato cha sita.
Erio anaomba Kamati hiyo katika shughuli zake iongeze na kazi ya udhibiti wa dawa za kulevya, kwakuwa anaamini sasa ni janga la kitaifa hususan kwa watu walio katika rika la ujana.

Monday, September 30, 2013

IKULU YA MULEBA HII HAPA:

hiyo nyumba inayoonekana mbele ndiyo Ikulu, iliyo upande wa kulia ni nyumba ya watu wa usalama.


Hivi ndivyo Ikulu ya Muleba inavyoonekana, Ndimo alimotakiwa kulala Rais na msafara wake

HUMU NDIMO MSAFARA WA RAIS JK ULIMOLALA, MULEBA, MKOANI KAGERA



Miongoni mwa mambo yaliyozua mjada mwaka huu nchini, ni ziara ya Rais Jakaya Kikwete  mkoani Kagera.

Pamoja na mengine, tukio la msafara wake kulala katika nyumba iliyoelezwa kuwa inamilikiwa na waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, badala ya kulala Ikulu ya mji wa Muleba; lilijadiliwa .
 
Sasa nawaletea picha za jengo alimolala Rais na msafara wake, lililopo Muleba. Baadaye nitawaletea picha ya jengo la Ikulu ya Mulega, walimotakiwa kulala.





Thursday, April 25, 2013

Wananchi wamechoka, kuwaongoza kunahitaji umakini


Matukio yanayoendelea kuibuka kila kukicha nchini, yakihusisha hali ya wananchi kutoridhishwa na matendo au maamuzi kadha wa kadha yanayofanywa na wanaowaongoza katika nyanja mbalimbali; ni ishara ya kuchoshwa na mazingira yanayowakabili.
Bila shaka ni ugumu wa maisha. Naamini hivyo ninapotafakari varangati lililojiri hivi karibuni Liwale, Mtwara.

Kwamba viongozi wa chama cha ushirika cha msingi Minali, walitaka kuwalipa Sh 200 kwa kilo moja wakulima waliowauzia Korosho kwa makubaliano ya kuwalipa Sh 1,200 kwa awamu. kwanza Sh 600 alafu Sh 600.
Mmoja wa viongozi hao alikaririwa na vyombo vya habari akisema makubaliano yalikuwa walipe kiasi hicho cha fedha kwa awamu.

Katika hali ya kawaida, ikiwa wakulima hao waliafiki makubaliano kiasi cha kutoa mazao yao kwa ushirika huo; ni dhahiri waliridhishwa na maelezo waliyopewa, hali inayotatiza kwanini wafanye vurugu kiasi cha kuteketeza mali za viongozi wao.
Mtazamo wangu unaniaminisha kuwa kuna mambo mawili; inawezekana chama kilieleza kuwa kingelipa Sh 600 kamili kwa awamu ya kwanza lakini Sh 600 ya kumalizia ingelipwa kwa awamu, huku wakulima wafikiri malipo yote yangefanywa kwa awamu mbili tu.

Au inawezekana viongozi wa ushirika walifikiri Tanzania ya leo ndiyo ile ya “jana na juzi”, wakataka kuchakachua na wakulima hawakukubali. Siyo rahisi mtu aliyeafiki kukupa mzigo na kupokea malipo ya awali, agome kupokea malipo ya mwisho na kufanya vurugu kubwa vile.
Ushauri

Inawezekana nikawa mdogo kiumri,madara na elimu kwa wanaoongoza umma wa Watanzania lakini nawaasa wasome alama za nyakati, wabadilike.
Hakuna anayependa kuona viongozi wakidharirishwa kwa mali zao kuchomwa moto, kutolewa matusi, kuzomewa ilhali wakiwa baba au mama wa Watanzania wenzetu lakini pia wanatakiwa kutambua kwamba Watanzania wengi wamekata tamaa.

Hakuna kitu kigumu na cha hatari chini ya jua kama kuongoza mtu aliyekata tamaa. Utasikia wakitupiana lawama, “mwanasiasa fulani ndiye amechochea, chama fulani ndicho kinataka nchi isitawalike...,” jamani! kuna mtu anayeweza kuambiwa ale mavi akayala?
Bila shaka hakuna, hivyo hali inayoendelea nchini haina budi kuwafikirisha viongozi wenye dhamana; kutambua kuwa muda wa kuongoza kwa kuahidi maendeleo bila matendo au kutekeleza maendeleo kwa mwendo wa kinyonga ili matatizo ya watu yaendelee kuwa mtaji wa wanasiasa umetutupa mkono.

Naipenda sana Tanzania, naipenda sana amani na ninatamani kuona mabadiliko kwa mtu mmoja mmoja na hatimaye jamii kwa ujumla. Mungu ibariki Tanzania.

 

 

Wednesday, April 17, 2013

CHIKU ABWAO NAYE ATEMA CHECHE BUNGENI


Chiku Abwao, viti maalumu (Chadema) anasema matusi, vurugu bungeni na kutikiswa kwa amani nchini kunatokana kunatokana na Chama Cha Mapinduzi, ambacho ni chama cha siasa kikongwe kuliko vyote nchini, kutosikiliza vilio vya wananchi.

Anasema wabunge wa kambi ya upinzani wanapoingia bungeni na kuwasilisha kiliio cha wapigakura wake, anazomewa, anabezwa na kuonekana hasemi lolote; matokeo yake nao wanajibu mapigo ndiyo maana bunge linaonekana kama ilivyo sasa.

(tofauti na zamani, sasa bunge limegubikwa na matumizi ya lugha za kukera na matusi hali inayosababisha kudhalilisha wahusika na taifa kwa ujumla)

Abwao anasema matukio ya watu kung’olewa kucha, meno na kujeruhiwa kwa namna tofauti kwanini yanawapata wanaoonekana kukosoa utendaji wa serikali?

Anasema hali hiyo ikihusishwa na hali iliyopo bungeni ambapo watu wanakosa uvumilivu hadharani kiasi cha hicho, inatia shaka watu hao wanapokuwa nje ya hadhara wanaweza kutenda mangapi.

MH. LEMA AMNYOOSHEA KIDOLE RAIS KUHUSU UDINI


Leo, Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema (Chadema) amesema bungeni kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, ndiye muasisi wa udini nchini.

Kauli hii iliwahi kurushwa hewani na blog hii kwamba ilitolewa na Kiongozi wa ngazi za juu wa chama cha CUF - taifa (bara) Julius Mtatilo; (rejea taarifa JK, CUF na Udini Tanania).

 Lema alishindwa kuendelea na uchangiaji wake katika eneo la aliloliita genge la usalama wa taifa linalong'oa watu kucha, meno na kuwatoboa macho raia kwa sababu wanazozijua wao.

 

PETER SELUKAMBA!!!!!!!


Leo Peter Selukamba (Mbunge Kigoma mjini (CCM) amefunga kazi ya matumizi ya matusi bungeni, baada ya kutoa tusi zito kuliko waliomtangulia.

Hayo yamejiri wakati akitaka kuonesha kuwa alichozungumza Tundu Lissu (Mb)kwamba msemaji wa kambi ya upinzani hakugusia kesi, wala ushahidi uliyotolewa katika kesi inayoendelea  mahakamani hakikuwa kweli.

Selukamba alikaririwa akisema, “Madai kwamba kambi ya  upinzani haikuzungumzia kesi iliyo mahakamani si yakweli, ukingalia ukurasa wa nne,” ikasikika mingong’ono iliyoashiria kutoridhishwa na alichokuwa akizungumza; mara sautiikasikika ikisema, “fuck you!”

Haya yanafanyika ndani ya Bunge, huku vyombo vya habari vikirusha matangazo ya moja kwa moja. inasikitisha, inatia aibu taifa.

Tanzania tutafaulu katika lipi? Elimu zii, kilimo zii, uchumi zii, michezo zii, ni kipi chenye manufaa kwa maisha yetu ya kila siku, tutakachofanya vizuri duniani? Kiongozi ni kioo cha jamii hivyo tunapowatazama viongozi bungeni ndipo tunapopata taswira ya jamii yetu.

Tujikague tumekwama wapi, tuchukue hatua la sivyo, tutaishia kulalama tu na mwisho wa siku hakuna la maana litakalotendeka zaidi ya kutukanana; wengine aina ya maisha yao ni matusi tosha unapomuingiza kwenye ulingo wa matusi inakuwa sawa na kumsukuma mlevi.

Friday, April 12, 2013

MABARAZA YA KATIBA MPYA YA TZ AU CHAMA FULANI?


Mwenzenu nimejionea maajabu kwenye uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya Katiba ngazi za wilaya.

Jaji Mkuu Mstaafu na Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya Katiba Tanzania, Joseph Warioba
Miongoni mwa wagombea wa nafasi hiyo, waliofika mbele ya Kamati ya maendeleo ya Kata ya Tabata inayoongozwa na diwani mwanamama Mtumwa, ni pamoja na wakili wa kujitegemea.

Bila shaka, alikusudia kutumia taaluma yake kuchangia mchakato wa taifa kujikwamua na changamoto nyingi zinazolikabili. ha! kwani Kamati ilijali uanasheria?!  Hakuchaguliwa bwana!
Waliochaguliwa kwa haraka ilibainika kuwa sifa ya kwanza na ya msingi ni wana chama kimoja tu. Kila mtu sasa anahoji ikiwa kinachokwenda kufanywa ni kupitia rasimu ya Katiba chama hicho au ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Saturday, April 6, 2013

ILALA YAITUNISHIA MISURI KAMATI YA BUNGE

Halmashauri ya manispaa ya Ilala imenyooshewa kidole na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) kwamba imeidharau.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbarouk  jana, wakati akitoa majumuisho ya mkutano kati yake na uongozi wa manispaa ya Kinondoni, kwenye ukumbi wa mikutano ndani ya ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam.
Mbarouk alisema kamati ilipofanya ziara wilayani humo ilipelekewa taarifa isiyokidhi viwango, wakaikataa na kutaka iandaliwe nyingine inayoonesha mapato na matumizi, madeni ambayo manispaa inadai na kudaiwa pamoja na mipango iliyopo inayotarajiwa kutekelezwa ili kujiletea maendeleo.
“Taarifa tuliyopewa ilikuwa ipoipo tu, imeandikwa kisiasa wakati sisi tunahitaji takwimu, siyo tu hawakutekeleza maelekezo tuliyowapa bali hata kwenye kikao hawakuja wala hawakuleta taarifa kwa katibu kama kanuni zinavyoelekeza, ikiwa kuna jambo limewatinga,” alieleza Mbarouk
Mbarouk alisema ziarani Ilala walishuhudia miradi yenye mambo mengi yanayotia shaka. Alitoa mfano wa mradi wa ujenzi wa eneo la ofisi za maofisa wa machinjio, unaloelezwa kugharimu Sh 14 mil.; ambao umetekelezwa bila kuzingatia taratibu za ununuzi wa umma.
“Nadhani mmeona ujenzi unaoendelea kwenye makutano ya barabara nyingi katikati ya jiji hili (Dar es Salaam) wanasiliba na mazege na kuweka bahari zisizokuwepo, michoro ya samaki na vinyago..., hatujaelewa wanakusudi gani maana wenzao maeneo kama hayo wanaweka bustani zenye maua mazuri,” alieleza Mbarouk na kuendelea
“Tulichofahamu ni kuwa gharama za ujenzi huo zinatolewa na wafadhili, hofu yetu ni ikiwa wafadhili hao ni walioweka mabango yao ya biashara, hii isije ikageuzwa njia ya kukwepa kulipa gharama za mabango ya matangazo maana ni moja ya vyanzo vya mapato ya halmashaur.”
Kufuatia hali hiyo, LAAC imeagiza halmashauri hiyo kupeleka mikataba yote ya miradi yake kwa CAG ili ikaguliwe na kuiwasilisha kwake kabla ya Aprili 12 mwaka huu, Dodoma.
Manispaa ya Kinondoni nayo ilitakiwa kudai haraka iwezekanavyo gawio lake kwenye uwekezaji unaofanywa kati yake na mbia Ohysterbey Villa, katika Kitalu 277 na 372.
Mbarouck alisema ikibidi halmashauri iombe kibali cha mahakama, kuzuia pato la mbia huyo, mpaka kesi ya msingi iliyopo mahakamani itakapomalizika.
Manispaa hiyo pia ilitakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inayochunguza suala la ununuzi wa Matela 27 ya kubebea taka ngumu, ili suala hilo likamilike haraka.

MWENDESHA MASHTAKA AMZINGUA KADA WA CHADEMA MAHAKAMANI

Mwendesha mashtaka amzingua kada wa Chadema
Kada wa Chadema, Gwakisa Barton amenusurika kuadhibiwa na mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, baada ya kushtukiwa na mwendesha mashtaka wa polisi, Inspekta Mathias Ezekia, akipiga picha wakati shughuli za mahakama zikiendelea.
Barton alifika mahakamani akiwa mmoja wa wana Chadema waliomsindikiza Mwenyekiti wa chama hicho jimboni Chalinze, Mathayo Torongei, anayetuhumiwa kuzuia karani wa uchaguzi Mwita Damsoni kufanya kazi yake katika uchaguzi wa viongozi wa kitongoji cha Kinyemvuu, Machi 3, mwaka huu.
Mara baada ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Frola Haule kuahirisha kesi ya Torongei, Inspekta Ezekiah alisikika akiomba mahakama iridhie kumpandisha kizimbani Barton, kwa kilichoelezwa kuwa alimpiga picha mahakama wakati mwenzake (Totongei) akiwa amesimama kizimbani.
Ombi hilo lilikubaliwa. Akiwa kizimbani, alihojiwa na hakimu Haule, “Kwanini usiadhibiwe kwa kupiga picha huku akifahamu kuwa ni kinyume cha taratibu za mahakama.
“Hapana mama yangu, sikupiga picha bali mheshimiwa alichoona ni mwanga uliotokea wakati nikiwasha simu, nilikuwa najiandaa kutoka nje baada ya shauri la mwenzangu kuahirishwa,” Gwakisa alijitetea.
Inspekta Ezekiah ili kupata ushahidi alitaka kupekua simu ya mtuhumiwa (Nokia N9) lakini alishindwa kutokana na kutofahamu matumizi yake. Jalada la kuhifadhi picha la simu hiyo lilifanikiwa kufunguliwa kwa msaada wa mmoja wa watu waliokuwa mahakamani hapo, ikathibitika hapakuwa na picha inayoonesha mandhari ya ndani ya mahakama. Mtuhumiwa aliachiwa huru
chanzo mwananchi ya leo.

Friday, April 5, 2013

KIMENUKA KWA JERRY SLAA!

                          Rajaba Mbarouk Mohammed
Hivi umeona ujenzi unaoendelea kwenye ‘round-about’ kadhaa katikati ya jiji la Dar es Salaam? kwa mfano unapokuwa barabara ya uhuru kuelekea mtaa wa kongo? Lile eneo limeenezwa makatuni, vinyago, limesakafiwa na kuchorwa michoro mfano wa bahari? Kama umeona ni vizuri ikiwa bado, nitapiga picha kisha niiweke uelewe ninachoeleza.

Sasa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) imeshtukia dili. Mwenyekiti wa LAAC, Rajaba Mbarouk Mohammed leo amesema wakiwa ziarani wilayani humo wameshtushwa na ujenzi huo. Mbali na kushutushwa na ubunifu huo ambao bado haijaeleweka unalenga nini, wamesikia gharama zake zinatolewa na ‘wafadhili’

Hoja ni kwamba, wafadhili hao wanafaidikaje? LAAC inawasiwasi kwamba, hiyo inaweza kuwa mbinu ya ama kukwepa kulipia mabango ya matangazo ya biashara; lakini kwakuwa manispaa hiyo imegoma kufika mbele ya kamati hiyo kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali likiwamo hilo, kama kamati hiyo ilivyoagiza, yote hayo bado ni kitendawili.

Thursday, April 4, 2013

RICHARD MBALASE NA VIJANA WAKE

Mwenyekiti wa Chadema wilayani Bagamoyo, Richard Mbalase (wa tatu)akiwa na ‘vijana wake’ Gwakisa (katikati)na Mathayo Torongei (wa kwanza) muda mfupi kabla ya kuingia ndani ya mahakama ya wilaya ya wilaya hiyo, ambamo kesi inayomkabili Torongei ilikuwa inatajwa kwa mara ya pili.

MPAMBANAJI WA CHADEMA JIMBONI CHALINZE KIZIMBANI BAGAMOYO

Mwenyekiti wa Chadema jimbo la Chalinze, Mathayo Torongei (benchi la pili, wa kwanza aliyevaa sare za chadema) akisubiri kupanda kizimbani katika mahakama ya wilaya ya Bagamoyo, jana, kujibu tuhuma za kumzuia karani wa uchaguzi Mwita Damson kufanya kazi yake, katika uchaguzi mdogo wa viongozi wa kitongoji cha Kinyemvuu, kijiji cha Kidomole jimboni Bagamoyo.
Upelelezi wa kesi hiyo ilielezwa kuwa umekamilika, itakuja tena 02 mwezi ujao, kusikilizwa.

Tuesday, April 2, 2013

CUF, JK NA UDINI TANZANIA

Naibu Katibu Mkuu wa CUF – Bara, Julius Mtatiro anasema Rais Jakaya Kikwete analia na mazao ya mimea aliyoipanda mwenyewe.
Anasema siyo siri kwamba taifa lipo katika hali mbaya kutokana na kukua kwa kasi kwa ubaguzi wenye vimelea vya udini; hali anayoielezea kuwa ni matokeo ya kampeini za baadhi ya wagombea, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, akiwamo Rais Jk
“Rais ni kati ya watu waliotumia Uislamu kuingia madarakani,” anaeleza Mtatiro. Alipohojiwa ikiwa ana ushahidi wa matamshi yake hayo, akasema “baada ya uchaguzi tulifanya uchambuzi na tukabaini njia kuu iliyomfanya apate wadhifa huo ni udini (uislamu).”
Akaelezwa kuwa bado hajasema ushahidi alionao, ndipo akasema “tunazo hotuba zake alizokuwa akitoa katika kampeini zake, zinabainisha kauli zake nyingi kubeba mbegu za udini, ambazo sasa zimechipua na kuathiri ustawi wa amani nchini”
Pamoja na JK, Mtatiro anawatuhumu wagombea wa uongozi kupitia CHADEMA kuwa nao walitumia Ukristo. Anamalizi kwa kusema, “hali itakuwa mbaya zaidi katika uchaguzi mkuu ujao, (2015) kwa sababu hali ikiendelea kuwa ilivyo, hatutashangaa kushuhudia wagombea wakichaguliwa kwa dini zao.”

Friday, March 22, 2013

WANAHABARI TUREJEE MAADILI


UANDISHI ni taaluma kama  nyingine. Ina maadili na kanuni zake. Moja ya maadili ambayo mwandishi anatakiwa kuzingatia ni  kutoingiza ushabiki katika kazi.
Miaka iliyopita, Abdallah Majura akitangaza moja ya  mechi, kati ya Simba na Yanga alishindwa kuficha mapenzi yake kwa timu anayoipenda. Aliibua gumzo mitaani.
Kisa cha kuibuka gumzo si kwamba jamii haifahamu kuwa ana chaguo lake, la hasha! bali maadili yalikuwa yakizingatia kwa kiwango cha kushtusha, ikitokea mtu akaonekana ameyakiuka.
hata Jane Mihanji alitekeleza rasmi hatua ya kuingia kwenye ulingo wa siasa, wengi walionekana kushtushwa kidogo kwa sababu awali maadili ya uandishi yalizuia kabisa kujihusisha na masuala yote ya aina hiyo.
Ingawa ni wazi kwamba kwasababu wanahabari ni wanadamu,  wana utashi na maono yao binafsi, wanatakiwa kuyaweka kando pindi wanapofanya kazi. Bila shaka hii ni kwa maslahi yao binafsi na jamii kwa ujumla.
Siamini kuwa waasisi wa misingi na maadili ya uanahabari hawakuwa na akili walipoamua hivyo.
Ukitafakari kwa kina utabaini kuwa walikuwa makini na wenye kuona mbali sana.
Maadili ya kazi hii yasipozingatiwa na chombo cha habari au mwanahabari mmojammoja dunia inaweza kugeuka mahala pasipo salama.
Leo tujiulize, tunafanya kazi zetu kwa kusimamia misingi ya uandishi wa habari? Bila shaka jibu ni hapana.
Kwanini? Hapa kila mmoja ana jawabu lake lakini kimsingi ninachoona ni njaa.
Ukihomi kwanini gazeti lenye hadhi ya kitaifa litoe toleo huku ukurasa wa mbele ukiwa umefunikwa na tangazo la Kampuni au biashara fulani, jibu litabaki kuwa ni njaa ya pesa.
 
Ukihoji kwa nini gazeti linalomilikiwa na chama cha siasa, litoe habari kuu ambayo kwa 100% ni kwa maslahi ya chama husika, jibu linabaki kwamba tatizo ni njaa, ya madaraka au fedha.
Jambo la kushangaza ni kwamba, vyombo hivyo vinaongozwa na wanataaluma waliobobea, wenye sifa na uzoefu wa kutosha. sasa kwanini hali iwe hivi? Jibu ni lile lile; njaa.
Kuna haja ya kubadili mwelekeo kitaaluma, misingi ya uandishi wa habari ni maadili. Naamini kila mtu anayeitwa mwanahabari anaifahamu sina haja ya kuitaja.
 

 

 

 

FASTJET NAO!

Mambo ya Fastjet bwana, mzigo usipodumbukia kwenye kiboksi hicho, andaa 8,000 ulipe tu. Hakuna longolongo.

ALAMA WANYOONESHA WANAMAANISHA...?


Heaven na Greyson sijui alama ya vidole wanayoonesha wanamaanisha ninachokifahamu??!! Godfrida kabaki na mshangao.