Tuesday, April 2, 2013

CUF, JK NA UDINI TANZANIA

Naibu Katibu Mkuu wa CUF – Bara, Julius Mtatiro anasema Rais Jakaya Kikwete analia na mazao ya mimea aliyoipanda mwenyewe.
Anasema siyo siri kwamba taifa lipo katika hali mbaya kutokana na kukua kwa kasi kwa ubaguzi wenye vimelea vya udini; hali anayoielezea kuwa ni matokeo ya kampeini za baadhi ya wagombea, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, akiwamo Rais Jk
“Rais ni kati ya watu waliotumia Uislamu kuingia madarakani,” anaeleza Mtatiro. Alipohojiwa ikiwa ana ushahidi wa matamshi yake hayo, akasema “baada ya uchaguzi tulifanya uchambuzi na tukabaini njia kuu iliyomfanya apate wadhifa huo ni udini (uislamu).”
Akaelezwa kuwa bado hajasema ushahidi alionao, ndipo akasema “tunazo hotuba zake alizokuwa akitoa katika kampeini zake, zinabainisha kauli zake nyingi kubeba mbegu za udini, ambazo sasa zimechipua na kuathiri ustawi wa amani nchini”
Pamoja na JK, Mtatiro anawatuhumu wagombea wa uongozi kupitia CHADEMA kuwa nao walitumia Ukristo. Anamalizi kwa kusema, “hali itakuwa mbaya zaidi katika uchaguzi mkuu ujao, (2015) kwa sababu hali ikiendelea kuwa ilivyo, hatutashangaa kushuhudia wagombea wakichaguliwa kwa dini zao.”

No comments:

Post a Comment