Saturday, April 6, 2013

ILALA YAITUNISHIA MISURI KAMATI YA BUNGE

Halmashauri ya manispaa ya Ilala imenyooshewa kidole na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) kwamba imeidharau.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbarouk  jana, wakati akitoa majumuisho ya mkutano kati yake na uongozi wa manispaa ya Kinondoni, kwenye ukumbi wa mikutano ndani ya ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam.
Mbarouk alisema kamati ilipofanya ziara wilayani humo ilipelekewa taarifa isiyokidhi viwango, wakaikataa na kutaka iandaliwe nyingine inayoonesha mapato na matumizi, madeni ambayo manispaa inadai na kudaiwa pamoja na mipango iliyopo inayotarajiwa kutekelezwa ili kujiletea maendeleo.
“Taarifa tuliyopewa ilikuwa ipoipo tu, imeandikwa kisiasa wakati sisi tunahitaji takwimu, siyo tu hawakutekeleza maelekezo tuliyowapa bali hata kwenye kikao hawakuja wala hawakuleta taarifa kwa katibu kama kanuni zinavyoelekeza, ikiwa kuna jambo limewatinga,” alieleza Mbarouk
Mbarouk alisema ziarani Ilala walishuhudia miradi yenye mambo mengi yanayotia shaka. Alitoa mfano wa mradi wa ujenzi wa eneo la ofisi za maofisa wa machinjio, unaloelezwa kugharimu Sh 14 mil.; ambao umetekelezwa bila kuzingatia taratibu za ununuzi wa umma.
“Nadhani mmeona ujenzi unaoendelea kwenye makutano ya barabara nyingi katikati ya jiji hili (Dar es Salaam) wanasiliba na mazege na kuweka bahari zisizokuwepo, michoro ya samaki na vinyago..., hatujaelewa wanakusudi gani maana wenzao maeneo kama hayo wanaweka bustani zenye maua mazuri,” alieleza Mbarouk na kuendelea
“Tulichofahamu ni kuwa gharama za ujenzi huo zinatolewa na wafadhili, hofu yetu ni ikiwa wafadhili hao ni walioweka mabango yao ya biashara, hii isije ikageuzwa njia ya kukwepa kulipa gharama za mabango ya matangazo maana ni moja ya vyanzo vya mapato ya halmashaur.”
Kufuatia hali hiyo, LAAC imeagiza halmashauri hiyo kupeleka mikataba yote ya miradi yake kwa CAG ili ikaguliwe na kuiwasilisha kwake kabla ya Aprili 12 mwaka huu, Dodoma.
Manispaa ya Kinondoni nayo ilitakiwa kudai haraka iwezekanavyo gawio lake kwenye uwekezaji unaofanywa kati yake na mbia Ohysterbey Villa, katika Kitalu 277 na 372.
Mbarouck alisema ikibidi halmashauri iombe kibali cha mahakama, kuzuia pato la mbia huyo, mpaka kesi ya msingi iliyopo mahakamani itakapomalizika.
Manispaa hiyo pia ilitakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inayochunguza suala la ununuzi wa Matela 27 ya kubebea taka ngumu, ili suala hilo likamilike haraka.

No comments:

Post a Comment