Friday, October 28, 2011

Mpende mtoto wako apendwe

Unafahamu kuna hali ya mtu kukataliwa na watu tena sababu za msingi. Kila anakokwenda anajikuta akichukiwa. Mathalani kazini, ndani ya familia hata ugenini.
Bila shaka hata wewe umewahi kushuhudia hali hiyo kwa ndugu, jamaa au rafiki na inawezekana hufahamu chanzo chake.
Ukweli ni kwamba, hiyo ni moja ya athari za tabia za wazazi, wanapokuwa katika hatua mbalimbali za kupata mtoto.
Matendo au maneno ya mzazi wakati mtoto akiwa tumboni mwa mama yake au hata kabla ya kutungwa mimba yana athari kubwa kwa mtoto na zaidi, anapozaliwa akiwa katika hatua tofauti za kukuzwa.
Inawezekana siyo suala geni kusika mzazi akisema ‘mimba ya mtoto huyu ilipatikana kwa bahati mbaya’ wengine hudiriki hata kuwatamkia watoto wao kwamba wamepatikana kwa bahati mbaya.
Mambo hayo ni chanzo cha watoto kuandamwa na hali ya kukataliwa katika jamii.
Hata kwa fikra ya kawaida, jambo hili linaleta mantiki kwa maana ikiwa mzazi uliyemleta mtoto duniani unathubutu kukiri kwamba amepatikana kwa bahati mbaya, nani atakubali kuwa naye kwa moyo mkunjufu?
Kwa vyovyote atachukiwa kila mahali na wakati mwingine hata yeye mwenyewe anaweza akikosa ujasiri wa kujipenda.
Ikiwa unamkumbuka au umewahi kusikia historia ya aliyekuwa Mbunge wa viti maalumu,  Hayati Amina Chifupa, utaungana nami kuwa ni mwanamke aliyekuwa akipendwa na watu wengi wa rika na jinsia tofauti.
Marehemu Amina Chifupa (Mb)

Ukifuatilia historia yake utabaini kuwa ni miongoni mwa watu waliokuzwa kwa kupendwa na kukubaliwa na wazazi wake.
Aidha yeye mwenyewe alikuwa mtu wa kujikubali na kujipenda. Akiwa hai, mwaka 2004 niliwahi kuzungumza naye kuhusu tabia yake ya kujipenda. 
Wakati tukiendelea na mazungumzo yetu, akafungua mkoba wake na kutoa kitambaa cha mkononi ambacho kilikuwa kimoja kati ya vitambaa vinne alivyokuwa amevihifadhi ndani ya  mkoba wake.
Vilikuwa vimetulia katika mpangilio mzuri na ndani ya mkoba wake huo mlikuwa na vitu vingi lakini vilivyo katika mpangilio mzuri unaovutia. Nikamsifia kwa umaridadi wake, ingawa ni vyema kila mwanamke akawa namna ile.
Alinijibu kwa kusema, “Editha, katika maisha yako yote usitamani kufanyiwa kitu ambacho wewe mwenyewe haujifanyii, mimi huwa naamini kwamba nikitaka kupendwa, sharti nijipende pia nikitaka kuaminiwa, nijiamini.”
Wakati nikiwaza mada ya malezi na makuzi wiki hii, nikakumbuka kauli zake nikaona si vibaya kuziweka bayana ili atakayeona mashiko yaliyo ndani yake, akazitumie kuwa mwongozo katika kufikia malengo aliyojiwekea maishani mwake.

Thursday, March 17, 2011

Hii ni ndoa au balaa maishani?!


Ninaye rafiki yangu wa siku nyingi, hivi karibuni amejifungua mtoto wake wa kwanza. Walipooana, miaka mitatu iliyopita, wakapanga nyumba Mbezi, jijini. Walijijengea desturi ya kushirikiana karibia katika kila kitu.
Wakakubaliana kudunduliza hela ya kodi ili mkataba ukiisha wasihangaike sana. Ikatunzwa wanakojua wenyewe. Ajabu kodi ilivyokwisha, mume akadai alipata tatizo binafsi akaitumia bila kumwambia mke.
Wakauza kabati la nguo na dressing table aliyozawadiwa mwanamke siku ya send-off. Kodi ikalipwa, wakaendelea. Sasa mwanamke amejifungua mtoto hajatimiza hata miezi mitatu, mwanaume akaiba vitenge vya wax vya mkewe, mke anaamini kuwa aliviuza kwa lengo la kunywa pombe, kwa sababu mwanaume ni chapombe.
Wakati varangati hilo halijaisha, kadi ya benki (ATM Card) ya bibie ikapotea, huku na huku, akakutwa nayo mwanaume kaificha. Akairejesha lakini mwanamke naye akakomaa ili arejeshewe na vitenge vyake. Akasema “Ukitaka tuelewane rudisha vitenge vyangu la, uende ukavitafute ulikovipeleka.”
Mke akaenda Clinic kurudi, mume kachukua nguo zake zote katokomea kusikojulikana! Leo hii siku ya tano. Hivi hii ni ndoa au ndoano? Ungekuwa wewe ndugu yangu ungefanyaje?
Acha maoni yako tafadhali.