Thursday, March 17, 2011

Hii ni ndoa au balaa maishani?!


Ninaye rafiki yangu wa siku nyingi, hivi karibuni amejifungua mtoto wake wa kwanza. Walipooana, miaka mitatu iliyopita, wakapanga nyumba Mbezi, jijini. Walijijengea desturi ya kushirikiana karibia katika kila kitu.
Wakakubaliana kudunduliza hela ya kodi ili mkataba ukiisha wasihangaike sana. Ikatunzwa wanakojua wenyewe. Ajabu kodi ilivyokwisha, mume akadai alipata tatizo binafsi akaitumia bila kumwambia mke.
Wakauza kabati la nguo na dressing table aliyozawadiwa mwanamke siku ya send-off. Kodi ikalipwa, wakaendelea. Sasa mwanamke amejifungua mtoto hajatimiza hata miezi mitatu, mwanaume akaiba vitenge vya wax vya mkewe, mke anaamini kuwa aliviuza kwa lengo la kunywa pombe, kwa sababu mwanaume ni chapombe.
Wakati varangati hilo halijaisha, kadi ya benki (ATM Card) ya bibie ikapotea, huku na huku, akakutwa nayo mwanaume kaificha. Akairejesha lakini mwanamke naye akakomaa ili arejeshewe na vitenge vyake. Akasema “Ukitaka tuelewane rudisha vitenge vyangu la, uende ukavitafute ulikovipeleka.”
Mke akaenda Clinic kurudi, mume kachukua nguo zake zote katokomea kusikojulikana! Leo hii siku ya tano. Hivi hii ni ndoa au ndoano? Ungekuwa wewe ndugu yangu ungefanyaje?
Acha maoni yako tafadhali.