Tuesday, October 29, 2013

UKAKASI KTK MIEZI 18 YA UTENDAJI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA




Novemba 1 mwaka, huu Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitimiza miezi 18 tangu ianze kazi za kuratibu mchakato wa Katiba. Ni wakati ambao ilitarajiwa iwe imewasilisha rasimu ya pili ya Katiba, kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa serikali ya Zanzibar.

Hatua hiyo haijatekelezwa, kutokana na ombi la tume hiyo kuongezewa mwezi mmoja, ili kukamilisha kazi hiyo na kuikabidhi kwa mamlaka husika. Hata hivyo, kumeibuka taarifa kwamba wajumbe wengi wa tume hiyo, wapo hatarini kiafya.


Hatari hiyo inaelezwa kutokana na ufinyu wa muda, ambao umepangwa bila kutilia maanani taratibu za kiafya, ikizingatiwa kuwa wengi wa wajumbe wa tume hiyo ni wenye umri usiopungua miaka 60
Kufuatia tetesi hizo, tukafuatilia ratiba ya utendaji wa tume hiyo, katika hatua inayotekelezwa; 
Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba

Kuboresha rasimu ya Katiba, kwa kutumia maoni yaliyotolewa na mabaraza ya Katiba ya wilaya zote nchini, taasisi, asasi na jumuiya zenye mtazamo unaofanana zisizopungua 600

Naibu Katibu wa tume, Casmir Kyuki anasema, 
“Tunafanya kazi siku zote za kazi including (ikiwamo) Jumapili, vikao vinaanza rasmi Saa 3: asubuhi mpaka Saa 7: tunapumzika kisha Saa 9: tunaendele; kumaliza inategemea na kundi limemaliza saa ngapi kwasababu wamegawanywa katika makundi; kwa mfano jana kuna walioondoka Saa 5: usiku.”

Daktari wa Afya ya binadamu, Dk. Joseph Masanja anasema mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 60 anapolazimika kufanya kazi ya kutumia zaidi akili, inatakiwa pamoja na mambo mengine, muda wa kufanya kazi uwe kati ya Saa Nne hadi Sita kwa siku; wenye umri chini ya huo wanaweza kufanya kazi kati ya Saa Sita hadi Nane kwa siku.

“Mazingira wanayofanyia kazi yanatakiwa yasiwe na viyoyozi (AC), kama ni lazima basi umakini unahitajika katika kuvitumia; Kinyume chake wataugua vichomi, (Pneumonia),” Dk. Dk.Masanja alisema

Dk.Masanja anasema kwa umri huo, mwili wa binadamu unakuwa katika hatari ya kushambuliwa na magonjwa, wengi wanakuwa  wanaugua Kisukari na Shinikizo la damu; kutozingatia umri, aina ya kazi na mazingira ni kuchochea magonjwa zaidi kwa muhusika.

“…, miili haishughulishwi vya kutosha, wafanye mazoezi sana ili mafuta yasijikusanye na kuganda kwenye mishipa, hali inayoweza kusababisha shinikizo la damu na hata kupooza mwili,” alieleza Dk. Masanja

Wajumbe hao wanaelezwa pia kuwa katika hatari ya kuugua ugonjwa utokanao na uchovu (fatique). Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na mtu kuwa na hasira za haraka, kukosa hamu ya kulala, kutolala usingizi vya kutosha au kukosa kabisa usingizi na mwili kuchoka.

Hata hivyo, mjumbe wa tume hiyo, Joseph Butiku alisema, “Fatigue ipo kila mahala, hata wewe unayetafuta na kuandika habari unaweza kuugua, hapa tunafanya kazi zetu kama kawaida tu, watu wengine wanapenda kukuza mambo.”

Jumamosi iliyopita, tulifika nyumbani kwa Mjumbe mwingine wa tume hiyo, John Nkolo, kumjulia hali baada ya kuugua akiwa kazini wilayani Sengerema, wakati tume ikiratibu maoni ya mabaraza ya Katiba ya wilaya.
Naibu Waziri wa Afya nchini, Dk. Seif Rashid

Baadaye uchunguzi wa madaktari ulibaini kuwa Nkolo, alipatwa na ugonjwa wa kupooza upande wa kulia; usoni na kwa maelezo ya mke wake, Joyce John, Daktari alisema ni bahati nzuri kwamba ubongo wake haukuathiriwa na ugonjwa huo. 

Sasa anafanya mazoezi ya viungo, ingawa hajaweza kuzungumza vizuri
 
Wiki mbili zilizopita, ziiliibuka tetesi kuwa afya ya Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba siyo nzuri na kwamba alikuwa nje ya nchi, kutibiwa. 

Tulimpigia simu yake ya kiganjani, ikapokewa na mwanamke aliyejitambulisha kuwa ni mke wake, akasema Jaji alikuwa nje ya nchi lakini hakuwa tayari kutaja nchi gani.

Mahojiano kati ya Mwandishi na Makamu mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Augustino Ramadhan, juu ya tetesi hizo yalifanyika hivi;
Mwandishi: Tuna taarifa kwamba afya ya mwenyekiti siyo nzuri, yupo nchini India akifanyiwa uchunguzi tunaomba kufahamu anavyoendelea.

Jaji Ramadhan: Eeeeh, mimi nipo Iringa, ila ni kweli mwenyekiti yupo India for checkup, (kuchunguzwa afya)ebu wasiliana na Katibu anaweza kukupa ufafanuzi zaidi.

Katibu wa tume, Assa Rashid hakupokea simu yake ya kiganjani kila alipopigiwa hali iliyosababisha atafutwe makamu wake,Casmir Kyuki;

“Nani amewaambia mwenyekiti yupo India?, Aliyewapa hizo taarifa kwanini asiwathibitishie? Kwani wewe ukienda Agha Khan kuonana na daktari, utakuwa mgonjwa?” alihoji Kyuki na kuendelea

“Yule (Jaji Warioba) kwa wadhifa wake (waziri mkuu mstaafu)anahudumiwa na serikali kuu na kwa umri wake siyo ajabu kuwa na utaratibu wa kufanyiwa checkup kila baada ya muda fulani, siyo mpaka augue; kwahiyo ikiwa yupo India labda ameenda kwa ajili hiyo.”

Mjumbe mwingine wa tume hiyo, Dk. Edimund Mvungi anasema, “Sioni kwanini mtu afiche ukweli uliyo wazi, tunafanya kazi kwa kasi ya ajabu; binafsi huwa naingia ofisini saa 12:45 kutoka inategemea muda wa kumaliza vikao…, wakati naingia tume nilikuwa na tatizo la Kisukari, Pressure imenianza nikiwa humu,” anaeleza Mvungi

Utafiti umebaini kuwa kwa muda wote huo, sera ya tume hiyo haina bima ya afya ya watendaji wake, mtu anapougua anatakiwa kujihudumia kisha kupeleka madai ili alipwe. 

Hoja ya msingi hapa ni; Watanzania watapata Katiba itakayowaletea matokeo wanayoyatarajia? Tukutane Juma lijalo, ambapo tutakuletea athari za hali hii katika ufanisi wa kazi.


Friday, October 25, 2013

PPF IMETUMIA 3 BIL KUSOMESHA YATIMA WA WANACHAMA WAKE



Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio, akizungumza kwenye mkutano na Kamati ya Bunge ya masuala ya UKIMWI
Mkurugenzi wa Mfuko wa Akiba wa PPF, William Erio akizungumza na Kamati ya Kudumu ya Bunge, ya masuala ya UKIMWI na dawa za kulevya leo, katika makao makuu ya mfuko huo jijini Dar es Salaam.

Mfuko huo kwa miaka 10 umeelezwa kutumia Sh. Bilioni 3 kusomesha watoto waliofiwa na wazazi wao, ambao walikuwa wananchama wake na tangu Januari mpaka Juni mwaka huu, Sh milioni 615 zimetumika kusomesha yatima 1,151; kuanzia chekechea hadi kidato cha nne.
Mwakani, mfuko huo utaongeza ufadhili huo kwa kusomesha watoto wa aina hiyo mpaka kidato cha sita.
Erio anaomba Kamati hiyo katika shughuli zake iongeze na kazi ya udhibiti wa dawa za kulevya, kwakuwa anaamini sasa ni janga la kitaifa hususan kwa watu walio katika rika la ujana.