Saturday, April 6, 2013

MWENDESHA MASHTAKA AMZINGUA KADA WA CHADEMA MAHAKAMANI

Mwendesha mashtaka amzingua kada wa Chadema
Kada wa Chadema, Gwakisa Barton amenusurika kuadhibiwa na mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, baada ya kushtukiwa na mwendesha mashtaka wa polisi, Inspekta Mathias Ezekia, akipiga picha wakati shughuli za mahakama zikiendelea.
Barton alifika mahakamani akiwa mmoja wa wana Chadema waliomsindikiza Mwenyekiti wa chama hicho jimboni Chalinze, Mathayo Torongei, anayetuhumiwa kuzuia karani wa uchaguzi Mwita Damsoni kufanya kazi yake katika uchaguzi wa viongozi wa kitongoji cha Kinyemvuu, Machi 3, mwaka huu.
Mara baada ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Frola Haule kuahirisha kesi ya Torongei, Inspekta Ezekiah alisikika akiomba mahakama iridhie kumpandisha kizimbani Barton, kwa kilichoelezwa kuwa alimpiga picha mahakama wakati mwenzake (Totongei) akiwa amesimama kizimbani.
Ombi hilo lilikubaliwa. Akiwa kizimbani, alihojiwa na hakimu Haule, “Kwanini usiadhibiwe kwa kupiga picha huku akifahamu kuwa ni kinyume cha taratibu za mahakama.
“Hapana mama yangu, sikupiga picha bali mheshimiwa alichoona ni mwanga uliotokea wakati nikiwasha simu, nilikuwa najiandaa kutoka nje baada ya shauri la mwenzangu kuahirishwa,” Gwakisa alijitetea.
Inspekta Ezekiah ili kupata ushahidi alitaka kupekua simu ya mtuhumiwa (Nokia N9) lakini alishindwa kutokana na kutofahamu matumizi yake. Jalada la kuhifadhi picha la simu hiyo lilifanikiwa kufunguliwa kwa msaada wa mmoja wa watu waliokuwa mahakamani hapo, ikathibitika hapakuwa na picha inayoonesha mandhari ya ndani ya mahakama. Mtuhumiwa aliachiwa huru
chanzo mwananchi ya leo.

No comments:

Post a Comment