Thursday, April 25, 2013

Wananchi wamechoka, kuwaongoza kunahitaji umakini


Matukio yanayoendelea kuibuka kila kukicha nchini, yakihusisha hali ya wananchi kutoridhishwa na matendo au maamuzi kadha wa kadha yanayofanywa na wanaowaongoza katika nyanja mbalimbali; ni ishara ya kuchoshwa na mazingira yanayowakabili.
Bila shaka ni ugumu wa maisha. Naamini hivyo ninapotafakari varangati lililojiri hivi karibuni Liwale, Mtwara.

Kwamba viongozi wa chama cha ushirika cha msingi Minali, walitaka kuwalipa Sh 200 kwa kilo moja wakulima waliowauzia Korosho kwa makubaliano ya kuwalipa Sh 1,200 kwa awamu. kwanza Sh 600 alafu Sh 600.
Mmoja wa viongozi hao alikaririwa na vyombo vya habari akisema makubaliano yalikuwa walipe kiasi hicho cha fedha kwa awamu.

Katika hali ya kawaida, ikiwa wakulima hao waliafiki makubaliano kiasi cha kutoa mazao yao kwa ushirika huo; ni dhahiri waliridhishwa na maelezo waliyopewa, hali inayotatiza kwanini wafanye vurugu kiasi cha kuteketeza mali za viongozi wao.
Mtazamo wangu unaniaminisha kuwa kuna mambo mawili; inawezekana chama kilieleza kuwa kingelipa Sh 600 kamili kwa awamu ya kwanza lakini Sh 600 ya kumalizia ingelipwa kwa awamu, huku wakulima wafikiri malipo yote yangefanywa kwa awamu mbili tu.

Au inawezekana viongozi wa ushirika walifikiri Tanzania ya leo ndiyo ile ya “jana na juzi”, wakataka kuchakachua na wakulima hawakukubali. Siyo rahisi mtu aliyeafiki kukupa mzigo na kupokea malipo ya awali, agome kupokea malipo ya mwisho na kufanya vurugu kubwa vile.
Ushauri

Inawezekana nikawa mdogo kiumri,madara na elimu kwa wanaoongoza umma wa Watanzania lakini nawaasa wasome alama za nyakati, wabadilike.
Hakuna anayependa kuona viongozi wakidharirishwa kwa mali zao kuchomwa moto, kutolewa matusi, kuzomewa ilhali wakiwa baba au mama wa Watanzania wenzetu lakini pia wanatakiwa kutambua kwamba Watanzania wengi wamekata tamaa.

Hakuna kitu kigumu na cha hatari chini ya jua kama kuongoza mtu aliyekata tamaa. Utasikia wakitupiana lawama, “mwanasiasa fulani ndiye amechochea, chama fulani ndicho kinataka nchi isitawalike...,” jamani! kuna mtu anayeweza kuambiwa ale mavi akayala?
Bila shaka hakuna, hivyo hali inayoendelea nchini haina budi kuwafikirisha viongozi wenye dhamana; kutambua kuwa muda wa kuongoza kwa kuahidi maendeleo bila matendo au kutekeleza maendeleo kwa mwendo wa kinyonga ili matatizo ya watu yaendelee kuwa mtaji wa wanasiasa umetutupa mkono.

Naipenda sana Tanzania, naipenda sana amani na ninatamani kuona mabadiliko kwa mtu mmoja mmoja na hatimaye jamii kwa ujumla. Mungu ibariki Tanzania.

 

 

No comments:

Post a Comment