Friday, March 8, 2013

Tanzania ina serikali?


Moja ya majukumu makuu ya serikali ni kuhakikishia kunakuwa na usalama kwa watu na mali zao.

Mambo yanayojiri kila kukicha nchini, yanalazimu mtu kuhoji ikiwa kuna serikali. Ikiwa ipo, ina hali gani? Hai, hoi?

Tafadhali msije kunichomoa kucha au kuning’oa meno na kunitenda vyovyote mtakavyo, lazima ukweli unaoniumiza mtima wangu, niuweke hadharani.

Tanzania inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya sheria. Kila raia amehakikishiwa haki ya kuishi na usalama wake kulindwa na serikali, kupitia vyombo vyake vya usalama; kwa mujibu wa Katiba.

Hivi leo kuna uhakika wa kuishi na kulindwa na vyombo vya dola nchini? Wakati raia wakivamiwa na kuteswa, wengine wakiuawa hadharani umma badala ya kuelezwa nani alihusika na hatua  gani zimechukuliwa dhidi yake, zinaundwa tume.

Baada ya Dk. Ulimboka Steven Ulimboka kutekwa, kupigwa, kung’olewa meno na kunyofolewa kucha kabla ya kuachwa msitu wa Pande afe, pamoja na yeye kuwapo na kuwa tayari kueleza au kutambua waliohusika; ikaundwa tume.

Tume inachunguza nini? Sasa amevamiwa Absalom Kibanda- Mhariri mtendaji wa New Habari Media Group – wachapisha ji wa magazeti ya Mtanzania, Rai na The African, yuko taabani kitandani; jeshi la polisi limeunda tume.

Hivi wananchi wakihisi au kuamini kuwa matukio haya yanafanywa na kundi Fulani lililo katika nafasi ya kuunda tume, likiwa limebuni njia hiyo kuwa moja ya njia za kujipatia fedha watakuwa wamekosea?

Kwanini tume? Jeshi la polisi bila tume haliwezi kufanya kazi? Mbona kamanda wa polisi mkoani Mwanza (Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi) Liberatus Barlow, alipouawa mbona polisi hawakuunda tume?

Tena ndani ya wiki mbili, watuhumiwa wote walikamatwa, mpaka vifaa vya mawasiliano alivyokuwa navyo kabla ya kuuawa pamoja na baadhi ya simu zilizokuwa zikitumiwa na watuhumiwa katika tukio hilo, zilipatikana kutoka kwenye shimo la choo; zilikofichwa.

Hii inamaanisha nini?

Kuna mgawanyo wa madaraja ya uhakika wa usalama kwa raia mbele ya dola la Tanzania?  Kwamba baadhi usalama wao upo kwa kiwango cha daraja A, wengine B, wengine C na hata Z!

Tafadhali msiniambie nimeandika habari za kichochezi, wachochezi na matendo ninayoeleza na lengo la kuyachambua ni kutaka dola yetu tukufu ibadilike.

Wahega walisema, mtoto wa mwenzio mbebe akiwa usingizini, akiamka habebeki. Kwa jinsi hali inavyoendelea, kuna kila sababu ya kuhoji uwapo wa serikali au mfano wa serikali nchini.

Ni mawazo yangu tu jamani, na wewe toa yako!

No comments:

Post a Comment