Sunday, March 10, 2013

JICHO LA KIBANDA JAMANI!

Haya sasa furahieni! Si ndivyo mlivyotaka mtoto wa wenzenu awe mlemavu? Aishi maisha yake yaliyobaki akiona kwa kutumia jicho moja? Furahieni basi!!!

Lakini mjue hukumu ya Mungu inawangoja. Hakina sina maneno yanayotosheleza kuwaelezea; kiasi gani mnakera.

Imefika wakati watu wanatamani kuwa wakimbia nchi yao? Mnaipeleka wapi Tanzania?

Hivi Absalom Kibanda, Dk. Steven Ulimboka, Saed Kubenea, Ndimara Tegambwage, Frederick Katulanda, Richard Mgamba na wengine wenye ushahidi kwamba wanatishiwa maisha na “watu wasiojulikana” wakiomba hifadhi nchi yoyote duniani;

Tanzania itabaki kwenye ramani ya nchi zenye ambani duniani? 

Hapo tunaweka kando vifo vilivyogubikwa utata vya kama vile cha Hayati Richard Massatu  na vingine vinavyodhaniwa kuwa vilitekelezwa wakati wa giza wakati kumbe ilikuwa hadharani tena mchana kweupe mbele ya macho za watu; kama kilichompata Hayati  Daudi Mwangosi.

Hivi amani inayohubiriwa, inayoagizwa kulindwa kwa nguvu na gharama zote ni ipi? Ni lini, wenye dhamana ya kusimamia amani watafumbua macho, kuona kuwa wajibu walioupokea kwa mikono miwili unamomonyoka mithiri ya barafu lililowekwa juani?

Nini kinasubiriwa kitokee, ili hatua zichukuliwe na zionekane machoni pa umma kuwa zinalengo la kukomesha uovu unaotendwa na makundi fulani, kwa maslahi yao binafsi na si kwa taifa?

Ndiyo, ni kwa maslahi binafsi kwa sababu ingekuwa ni kwa maslahi ya taifa, vyombo vya kutetea maslahi ya aina hiyo; mathalan mahakama na mamlaka zinazosimamia taaluma nchini zipo, kwanini zisitumike?

Kwanini iwe kukomoana kwa kunyofoa viungo, kupigana na hata kuripua kwa mabomu raia wasio hatia kwa mujibu wa sheria za nchi; kisa kundi moja lina uwezo wa kifedha au dhamana kuliko jingine?
Inaboa sana aisee! Achene hizo.

No comments:

Post a Comment