Monday, March 4, 2013

Kila mke angefurahi kuwa na mume wa aina hii
Anaitwa Emmanuel Mmari, ni mchaga wa Siha, Sanya juu wilayani. Siyo kwamba amekimbiwa na mke na kuterkezewa mtoto, la hasha! Ni mwanaume mwenye sifa ya Baba au mume mwema.
Mmari siyo kwamba hana kazi ndiyo maana anamsaidia mke wake kubeba mtoto anapokuwa na safari za kifamilia, la hasha! ni dereva wa gari kubwa linalosafirisha nishati ya mafuta ndani na nje ya nchi, almaarufu semi tela.
Nilimkuta ameketi nje ya Duka la Magodoro, Kariakoo mtaa wa Uhuru akiwa amempakata mtoto wake anayemtaja kwa jina la Angel , mwenye umri wa miezi miwili. Mama yake inaelezwa na Mmari  kuwa alikuwa ameingia ndani ya mitaa ya  Kariakoo, kununua hereni za mtoto wao.

“Mimi sijawa na uwezo wa kumnunulia mke wangu gari, siwezi kumuacha apande daladala peke yake huku amebeba mtoto wetu aje kununua vifaa na bidhaa za nyumbani, huwa namsindikiza na hata alipokuwa mjamzito nilikuwa nikienda naye kliniki,” Mmari anaeleza.
Wanaishi Bomubomu- Kiwaloani, wilayani Temeke. Mkewe pia ni Mchaga wa Kiboroloni. Walikuwa wamekwenda Kariakoo kununua godoro na vifaa mbalimbali vya nyumbani.
Mmari anatoa wito kwa vijana wenzake kwamba, wanapoamua kuanzisha familia kwa kuoa na kuwa na watoto, wawe bega kwa bega na wake zao kujenga familia bora badala ya kutegemea mke afanye kila kitu, kwa kisingizio cha mume kutafuta fedha.
Hongera sana Mmari, u baba, mume wa kuigwa

No comments:

Post a Comment