Tuesday, March 26, 2013
Friday, March 22, 2013
WANAHABARI TUREJEE MAADILI
UANDISHI
ni taaluma kama nyingine. Ina maadili na kanuni zake. Moja ya
maadili ambayo mwandishi anatakiwa kuzingatia ni kutoingiza ushabiki
katika kazi.
Miaka iliyopita, Abdallah Majura akitangaza moja ya mechi, kati ya Simba na
Yanga alishindwa kuficha mapenzi yake kwa timu anayoipenda. Aliibua gumzo mitaani.
Kisa cha kuibuka gumzo si kwamba jamii haifahamu kuwa ana chaguo lake, la hasha! bali maadili yalikuwa yakizingatia kwa kiwango cha kushtusha, ikitokea mtu akaonekana ameyakiuka.
hata Jane Mihanji alitekeleza rasmi hatua ya kuingia kwenye ulingo wa siasa, wengi walionekana kushtushwa kidogo kwa sababu awali maadili ya uandishi yalizuia kabisa kujihusisha na masuala yote ya aina hiyo.
Ingawa ni wazi kwamba kwasababu wanahabari ni wanadamu, wana utashi na maono yao
binafsi, wanatakiwa kuyaweka kando pindi wanapofanya kazi. Bila shaka hii ni kwa maslahi yao
binafsi na jamii kwa ujumla.
Siamini kuwa
waasisi wa misingi na maadili ya uanahabari hawakuwa na akili walipoamua hivyo.
Ukitafakari kwa kina utabaini kuwa walikuwa makini na wenye kuona mbali sana.
Maadili ya
kazi hii yasipozingatiwa na chombo cha habari au mwanahabari
mmojammoja dunia inaweza kugeuka mahala pasipo salama.
Leo tujiulize,
tunafanya kazi zetu kwa kusimamia misingi ya uandishi wa habari? Bila shaka
jibu ni hapana.
Kwanini? Hapa kila mmoja ana jawabu lake lakini kimsingi
ninachoona ni njaa.
Ukihomi kwanini
gazeti lenye hadhi ya kitaifa litoe toleo huku ukurasa wa mbele ukiwa
umefunikwa na tangazo la Kampuni au biashara fulani, jibu litabaki kuwa ni njaa
ya pesa.
Ukihoji kwa
nini gazeti linalomilikiwa na chama cha siasa, litoe habari kuu
ambayo kwa 100% ni kwa maslahi ya chama husika, jibu linabaki kwamba tatizo ni njaa, ya madaraka au fedha.
Jambo la kushangaza ni kwamba, vyombo hivyo vinaongozwa na wanataaluma waliobobea, wenye sifa na
uzoefu wa kutosha. sasa kwanini hali iwe hivi? Jibu ni lile lile;
njaa.
Kuna haja
ya kubadili mwelekeo kitaaluma, misingi ya uandishi wa habari
ni maadili. Naamini kila mtu anayeitwa mwanahabari anaifahamu sina
haja ya kuitaja.
MWANZA NAKO HAYA YAPO
Jamaa nusura amchape vibao mmoja wa
waliofunga gari lake kwa madai kwamba limeegeshwa sehemu ya watembea kwa miguu,
nje ya Hoteli ya Mwanza; jijini Mwanza.
Baada ya wanahabari kuingilia kati
, ikabainika ilikuwa ubabaishaji kwani baada ya waliofunga kuhojiwa
kwanini wamefunga gari moja wakati yaliyoegeshwa ni mengi, hakukuwa na majibu ya
msingi; wakalifungua baba wa watu akasepa zake.
Wednesday, March 20, 2013
Thursday, March 14, 2013
Baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya Muungano wa Utepe
Mweupe Tanzania, waliotokea makao makuu Dar es Salaam; wakiwa ofisini kwa
Mganga mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Valentino Bangi (aliyekaa nyuma ya meza yenye mafaili
mengi) wakipanga mikakati ya kufanikisha siku ya maadhimisho ya uzazi salama
duniani, kitaifa mwaka huu yanaadhimishwa kesho jijini Mwanza.
SALUM Charles (8) anayesoma darasa la kwanza shule ya Msingi
Nyamagana, jijini Mwanza bila kufahamu kuwa anaozungumza nao ni madaktari, (Dk.
Koheleth Winani na Dk. Ahmed Makuwani) akieleza kuwa anasoma kwa bidii ili
baadaye awe Daktari atakayefundisha watu wasiugue ovyo. Madaktari kwa furaha walimpa
Sh 3000 akanunue kalamu na daftari wakimtia moyo aongeze bidii ili atimize
ndoto zake.
Sunday, March 10, 2013
JICHO LA KIBANDA JAMANI!
Haya sasa furahieni! Si ndivyo mlivyotaka mtoto wa wenzenu awe mlemavu? Aishi maisha yake yaliyobaki akiona kwa kutumia jicho moja? Furahieni basi!!!
Lakini mjue hukumu ya Mungu inawangoja. Hakina sina maneno yanayotosheleza kuwaelezea; kiasi gani mnakera.
Imefika wakati watu wanatamani kuwa wakimbia nchi yao? Mnaipeleka wapi Tanzania?
Hivi Absalom Kibanda, Dk. Steven Ulimboka, Saed Kubenea, Ndimara Tegambwage, Frederick Katulanda, Richard Mgamba na wengine wenye ushahidi kwamba wanatishiwa maisha na “watu wasiojulikana” wakiomba hifadhi nchi yoyote duniani;
Tanzania itabaki kwenye ramani ya nchi zenye ambani duniani?
Hapo tunaweka kando vifo vilivyogubikwa utata vya kama vile cha Hayati Richard Massatu na vingine vinavyodhaniwa kuwa vilitekelezwa wakati wa giza wakati kumbe ilikuwa hadharani tena mchana kweupe mbele ya macho za watu; kama kilichompata Hayati Daudi Mwangosi.
Hivi amani inayohubiriwa, inayoagizwa kulindwa kwa nguvu na gharama zote ni ipi? Ni lini, wenye dhamana ya kusimamia amani watafumbua macho, kuona kuwa wajibu walioupokea kwa mikono miwili unamomonyoka mithiri ya barafu lililowekwa juani?
Nini kinasubiriwa kitokee, ili hatua zichukuliwe na zionekane machoni pa umma kuwa zinalengo la kukomesha uovu unaotendwa na makundi fulani, kwa maslahi yao binafsi na si kwa taifa?
Ndiyo, ni kwa maslahi binafsi kwa sababu ingekuwa ni kwa maslahi ya taifa, vyombo vya kutetea maslahi ya aina hiyo; mathalan mahakama na mamlaka zinazosimamia taaluma nchini zipo, kwanini zisitumike?
Kwanini iwe kukomoana kwa kunyofoa viungo, kupigana na hata kuripua kwa mabomu raia wasio hatia kwa mujibu wa sheria za nchi; kisa kundi moja lina uwezo wa kifedha au dhamana kuliko jingine?
Inaboa sana aisee! Achene hizo.
Friday, March 8, 2013
Tanzania ina serikali?
Moja ya majukumu makuu ya serikali ni kuhakikishia kunakuwa na usalama kwa watu na mali zao.
Mambo yanayojiri kila kukicha nchini, yanalazimu mtu kuhoji ikiwa kuna serikali. Ikiwa ipo, ina hali gani? Hai, hoi?
Tafadhali msije kunichomoa kucha au kuning’oa meno na kunitenda vyovyote mtakavyo, lazima ukweli unaoniumiza mtima wangu, niuweke hadharani.
Tanzania inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya sheria. Kila raia amehakikishiwa haki ya kuishi na usalama wake kulindwa na serikali, kupitia vyombo vyake vya usalama; kwa mujibu wa Katiba.
Hivi leo kuna uhakika wa kuishi na kulindwa na vyombo vya dola nchini? Wakati raia wakivamiwa na kuteswa, wengine wakiuawa hadharani umma badala ya kuelezwa nani alihusika na hatua gani zimechukuliwa dhidi yake, zinaundwa tume.
Baada ya Dk. Ulimboka Steven Ulimboka kutekwa, kupigwa, kung’olewa meno na kunyofolewa kucha kabla ya kuachwa msitu wa Pande afe, pamoja na yeye kuwapo na kuwa tayari kueleza au kutambua waliohusika; ikaundwa tume.
Tume inachunguza nini? Sasa amevamiwa Absalom Kibanda- Mhariri mtendaji wa New Habari Media Group – wachapisha ji wa magazeti ya Mtanzania, Rai na The African, yuko taabani kitandani; jeshi la polisi limeunda tume.
Hivi wananchi wakihisi au kuamini kuwa matukio haya yanafanywa na kundi Fulani lililo katika nafasi ya kuunda tume, likiwa limebuni njia hiyo kuwa moja ya njia za kujipatia fedha watakuwa wamekosea?
Kwanini tume? Jeshi la polisi bila tume haliwezi kufanya kazi? Mbona kamanda wa polisi mkoani Mwanza (Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi) Liberatus Barlow, alipouawa mbona polisi hawakuunda tume?
Tena ndani ya wiki mbili, watuhumiwa wote walikamatwa, mpaka vifaa vya mawasiliano alivyokuwa navyo kabla ya kuuawa pamoja na baadhi ya simu zilizokuwa zikitumiwa na watuhumiwa katika tukio hilo, zilipatikana kutoka kwenye shimo la choo; zilikofichwa.
Hii inamaanisha nini?
Kuna mgawanyo wa madaraja ya uhakika wa usalama kwa raia mbele ya dola la Tanzania? Kwamba baadhi usalama wao upo kwa kiwango cha daraja A, wengine B, wengine C na hata Z!
Tafadhali msiniambie nimeandika habari za kichochezi, wachochezi na matendo ninayoeleza na lengo la kuyachambua ni kutaka dola yetu tukufu ibadilike.
Wahega walisema, mtoto wa mwenzio mbebe akiwa usingizini, akiamka habebeki. Kwa jinsi hali inavyoendelea, kuna kila sababu ya kuhoji uwapo wa serikali au mfano wa serikali nchini.
Ni mawazo yangu tu jamani, na wewe toa yako!
Thursday, March 7, 2013
Tuesday, March 5, 2013
Songas hawezi kugoma kuuzia umeme Tanesco
KATIBU Mkuu wa wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amesema Songas, (mwekezaji anayezalisha umeme na kuuzia Tanesco) hana uwezo wa kugoma kuliuzia shirika hilo umeme.
Kauli hiyo ilitokana na taarifa kwamba Tanesco limelemewa na mzigo wa madeni, kiasi cha kushindwa kujiendesha huku baadhi ya wawekezaji wakitishia kusitisha kuliuzia umeme.
Songas, ambayo taarifa mbalimbali zinasema inaidai Tanesco Sh 80 bilioni, ilitajwa na Maswi kwamba nayo inadaiwa na serikali dola za Marekani 10.4 milioni, sawa na Sh16.64 bilioni.
“Songas hana ubavu kuzima mitambo maana siyo mmiliki pekee wa mitambo hiyo; serikali kupitia TPDC na Tanesco inamiliki asilimia 29 ya hisa za uwekezaji ukiachilia mbali anayeendesha mitambo kampuni ya Pan African,” alieleza Maswi. Alisema serikali itamlipa lakini itakata fedha zake inazomdai.
Monday, March 4, 2013
Kila mke angefurahi kuwa na mume wa aina hii
Anaitwa Emmanuel Mmari, ni mchaga wa Siha, Sanya juu wilayani. Siyo kwamba amekimbiwa na mke na kuterkezewa mtoto, la hasha! Ni mwanaume mwenye sifa ya Baba au mume mwema.
Mmari siyo kwamba hana kazi ndiyo maana anamsaidia mke wake kubeba mtoto anapokuwa na safari za kifamilia, la hasha! ni dereva wa gari kubwa linalosafirisha nishati ya mafuta ndani na nje ya nchi, almaarufu semi tela.
Nilimkuta ameketi nje ya Duka la Magodoro, Kariakoo mtaa wa Uhuru akiwa amempakata mtoto wake anayemtaja kwa jina la Angel , mwenye umri wa miezi miwili. Mama yake inaelezwa na Mmari kuwa alikuwa ameingia ndani ya mitaa ya Kariakoo, kununua hereni za mtoto wao.
Wanaishi Bomubomu- Kiwaloani, wilayani Temeke. Mkewe pia ni Mchaga wa Kiboroloni. Walikuwa wamekwenda Kariakoo kununua godoro na vifaa mbalimbali vya nyumbani.
Mmari anatoa wito kwa vijana wenzake kwamba, wanapoamua kuanzisha familia kwa kuoa na kuwa na watoto, wawe bega kwa bega na wake zao kujenga familia bora badala ya kutegemea mke afanye kila kitu, kwa kisingizio cha mume kutafuta fedha.
Hongera sana Mmari, u baba, mume wa kuigwa
Tume kufuatilia anguko la mitihani ya Kidato cha Nne
Hivi karibuni Waziri mkuu Mizengo Pinda ameunda tume inayoongozwa na Profesa Sifuni Mchome, eti kutafuta suluhisho la matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne nchini.
Kumbukumbu zinaonesha utafiti wa aina hiyo umewahi kufanywa mwaka 2010, matokeo yake yaliwasilishwa serikalini na kuna mapendekezo ambayo yalitokana na utafiti huo, lakini hakuna hata moja lililotekelezwa.
Watanzania tujiulize, tume hizi mpaka lini? Fedha kiasi gani zinatumika kulipa wajumbe wa tume, kuiwezesha kutekeleza majukumu wanayopewa? Naamini fedha hizo zingetumika kutekeleza moja au baadhi ya mapendekezo yaliyowahi kutolewa katika tafiti lizowahi kufanywa, nchi ingepiga hatua kielimu.
Muda wa blablaa umepita, serikali na watendaji achene kuchezea fikra za wananchi tuliowapa dhamana badala yake tekelezeni majukumu yenu kwa dhamira safi ama sivyo, vizazi vijavyo vitawahukumu na pengine kuchapa viboko makaburi yenu.
Huu ni mtazamo wangu tu.
Friday, March 1, 2013
Wizi wa dawa za serikali:
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) Cosmas Mwaifwani, akizungumza kwenye kongamano la kihabari lililoandaliwa na Mfuko wa Bima wa Taifa (NHIF)mkoani Mtwara alisema,"Kila mkoa kuna kesi angalau moja ya wizi wa dawa za serikali inayomkabiri mtumishi wa serikali."
Akasimulia tukio ambalo gari la MSD lilikutwa likiteremsha dawa kwenye nyumba ya mtu binafsi, tena iliyo jirani na kituo cha polisi.
Akasema hata baada ya taarifa kufikishwa kituo cha polisi, ilichukua saa tatu kwa polisi kufika, tena walikamatwa baada ya TAKUKURU kupelekewa taarifa na kuingilia kati.
"Dereva wetu aliyehusika tulimfukuza kazi lakini alirudishwa na watuhumiwa wengine mpaka leo wapo uraiani," hiyo ni kauli ya Mwaifwani
Anasema kutokana na uzoefu alionao, kesi zote za aina hiyo serikali haishindi.
ebu toa maoni yako katika hili!
Subscribe to:
Posts (Atom)