Friday, March 8, 2013

Tanzania ina serikali?


Moja ya majukumu makuu ya serikali ni kuhakikishia kunakuwa na usalama kwa watu na mali zao.

Mambo yanayojiri kila kukicha nchini, yanalazimu mtu kuhoji ikiwa kuna serikali. Ikiwa ipo, ina hali gani? Hai, hoi?

Tafadhali msije kunichomoa kucha au kuning’oa meno na kunitenda vyovyote mtakavyo, lazima ukweli unaoniumiza mtima wangu, niuweke hadharani.

Tanzania inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya sheria. Kila raia amehakikishiwa haki ya kuishi na usalama wake kulindwa na serikali, kupitia vyombo vyake vya usalama; kwa mujibu wa Katiba.

Hivi leo kuna uhakika wa kuishi na kulindwa na vyombo vya dola nchini? Wakati raia wakivamiwa na kuteswa, wengine wakiuawa hadharani umma badala ya kuelezwa nani alihusika na hatua  gani zimechukuliwa dhidi yake, zinaundwa tume.

Baada ya Dk. Ulimboka Steven Ulimboka kutekwa, kupigwa, kung’olewa meno na kunyofolewa kucha kabla ya kuachwa msitu wa Pande afe, pamoja na yeye kuwapo na kuwa tayari kueleza au kutambua waliohusika; ikaundwa tume.

Tume inachunguza nini? Sasa amevamiwa Absalom Kibanda- Mhariri mtendaji wa New Habari Media Group – wachapisha ji wa magazeti ya Mtanzania, Rai na The African, yuko taabani kitandani; jeshi la polisi limeunda tume.

Hivi wananchi wakihisi au kuamini kuwa matukio haya yanafanywa na kundi Fulani lililo katika nafasi ya kuunda tume, likiwa limebuni njia hiyo kuwa moja ya njia za kujipatia fedha watakuwa wamekosea?

Kwanini tume? Jeshi la polisi bila tume haliwezi kufanya kazi? Mbona kamanda wa polisi mkoani Mwanza (Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi) Liberatus Barlow, alipouawa mbona polisi hawakuunda tume?

Tena ndani ya wiki mbili, watuhumiwa wote walikamatwa, mpaka vifaa vya mawasiliano alivyokuwa navyo kabla ya kuuawa pamoja na baadhi ya simu zilizokuwa zikitumiwa na watuhumiwa katika tukio hilo, zilipatikana kutoka kwenye shimo la choo; zilikofichwa.

Hii inamaanisha nini?

Kuna mgawanyo wa madaraja ya uhakika wa usalama kwa raia mbele ya dola la Tanzania?  Kwamba baadhi usalama wao upo kwa kiwango cha daraja A, wengine B, wengine C na hata Z!

Tafadhali msiniambie nimeandika habari za kichochezi, wachochezi na matendo ninayoeleza na lengo la kuyachambua ni kutaka dola yetu tukufu ibadilike.

Wahega walisema, mtoto wa mwenzio mbebe akiwa usingizini, akiamka habebeki. Kwa jinsi hali inavyoendelea, kuna kila sababu ya kuhoji uwapo wa serikali au mfano wa serikali nchini.

Ni mawazo yangu tu jamani, na wewe toa yako!

Thursday, March 7, 2013


Ee Mungu nakuomba umponye mapema ndugu yetu Kibanda, arejee katika hali yake ya afya njema. Amina.

Tuesday, March 5, 2013

Songas hawezi kugoma kuuzia umeme Tanesco


KATIBU Mkuu wa wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amesema Songas, (mwekezaji anayezalisha umeme na kuuzia Tanesco) hana uwezo wa kugoma kuliuzia shirika hilo umeme.

Kauli hiyo ilitokana na taarifa kwamba Tanesco limelemewa na mzigo wa madeni, kiasi cha kushindwa kujiendesha huku baadhi ya wawekezaji wakitishia kusitisha kuliuzia umeme.

Songas, ambayo taarifa mbalimbali zinasema inaidai Tanesco Sh 80 bilioni, ilitajwa na Maswi kwamba  nayo inadaiwa na serikali dola za Marekani 10.4 milioni, sawa na Sh16.64 bilioni.

“Songas hana ubavu kuzima mitambo maana siyo mmiliki pekee wa mitambo hiyo; serikali kupitia TPDC na Tanesco inamiliki asilimia 29 ya hisa za uwekezaji ukiachilia mbali anayeendesha mitambo kampuni ya Pan African,” alieleza Maswi. Alisema serikali itamlipa lakini itakata fedha zake inazomdai.

Monday, March 4, 2013

Kila mke angefurahi kuwa na mume wa aina hii
Anaitwa Emmanuel Mmari, ni mchaga wa Siha, Sanya juu wilayani. Siyo kwamba amekimbiwa na mke na kuterkezewa mtoto, la hasha! Ni mwanaume mwenye sifa ya Baba au mume mwema.
Mmari siyo kwamba hana kazi ndiyo maana anamsaidia mke wake kubeba mtoto anapokuwa na safari za kifamilia, la hasha! ni dereva wa gari kubwa linalosafirisha nishati ya mafuta ndani na nje ya nchi, almaarufu semi tela.
Nilimkuta ameketi nje ya Duka la Magodoro, Kariakoo mtaa wa Uhuru akiwa amempakata mtoto wake anayemtaja kwa jina la Angel , mwenye umri wa miezi miwili. Mama yake inaelezwa na Mmari  kuwa alikuwa ameingia ndani ya mitaa ya  Kariakoo, kununua hereni za mtoto wao.

“Mimi sijawa na uwezo wa kumnunulia mke wangu gari, siwezi kumuacha apande daladala peke yake huku amebeba mtoto wetu aje kununua vifaa na bidhaa za nyumbani, huwa namsindikiza na hata alipokuwa mjamzito nilikuwa nikienda naye kliniki,” Mmari anaeleza.
Wanaishi Bomubomu- Kiwaloani, wilayani Temeke. Mkewe pia ni Mchaga wa Kiboroloni. Walikuwa wamekwenda Kariakoo kununua godoro na vifaa mbalimbali vya nyumbani.
Mmari anatoa wito kwa vijana wenzake kwamba, wanapoamua kuanzisha familia kwa kuoa na kuwa na watoto, wawe bega kwa bega na wake zao kujenga familia bora badala ya kutegemea mke afanye kila kitu, kwa kisingizio cha mume kutafuta fedha.
Hongera sana Mmari, u baba, mume wa kuigwa

Tume kufuatilia anguko la mitihani ya Kidato cha Nne
Hivi karibuni Waziri mkuu Mizengo Pinda ameunda tume inayoongozwa na Profesa Sifuni Mchome, eti kutafuta suluhisho la matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne nchini.
Kumbukumbu zinaonesha utafiti wa aina hiyo umewahi kufanywa mwaka 2010, matokeo yake yaliwasilishwa serikalini na kuna mapendekezo ambayo yalitokana na utafiti huo, lakini hakuna hata moja lililotekelezwa.
Watanzania tujiulize, tume hizi mpaka lini? Fedha kiasi gani zinatumika kulipa wajumbe wa tume, kuiwezesha kutekeleza majukumu wanayopewa? Naamini fedha hizo zingetumika kutekeleza moja au baadhi ya mapendekezo yaliyowahi kutolewa katika tafiti lizowahi kufanywa, nchi ingepiga hatua kielimu.
Muda wa blablaa umepita, serikali na watendaji achene kuchezea fikra za wananchi tuliowapa dhamana badala yake tekelezeni majukumu yenu kwa dhamira safi ama sivyo, vizazi vijavyo vitawahukumu na pengine kuchapa viboko makaburi yenu.
Huu ni mtazamo wangu tu.

Friday, March 1, 2013

Wizi wa dawa za serikali:
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) Cosmas Mwaifwani, akizungumza kwenye kongamano la kihabari lililoandaliwa na Mfuko wa Bima wa Taifa (NHIF)mkoani Mtwara alisema,"Kila mkoa kuna kesi angalau moja ya wizi wa dawa za serikali inayomkabiri mtumishi wa serikali."
Akasimulia tukio ambalo gari la MSD lilikutwa likiteremsha dawa kwenye nyumba ya mtu binafsi, tena iliyo jirani na kituo cha polisi.
Akasema hata baada ya taarifa kufikishwa kituo cha polisi, ilichukua saa tatu kwa polisi kufika, tena walikamatwa baada ya TAKUKURU kupelekewa taarifa na kuingilia kati.
"Dereva wetu aliyehusika tulimfukuza kazi lakini alirudishwa na watuhumiwa wengine mpaka leo wapo uraiani," hiyo ni kauli ya  Mwaifwani
Anasema kutokana na uzoefu alionao, kesi zote za aina hiyo serikali haishindi.
ebu toa maoni yako katika hili!

Thursday, February 28, 2013

UNAFAHAMU?
Wizi wa dawa serikalini ni changamoto kubwa kwa utekelezaji wenye ufanisi wa Bohari Kuu ya Dawa Tanzania (MSD)?
nitakuletea alichodokeza mkurugenzi wa MSD kuhusu hilo
 
Usiyoyajua kuhusu MSD
Je, unafahamu Bohari kuu ya Dawa Tanzania (MSD) hununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara  kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma ya afya nchini kutoka vyanzo gani?
Pata taarifa kama haufahamu;
Dawa: asilimia 80% huagizwa kutoka nje ya nchi
Vifaa tiba: asilimia 95% huagizwa kutoka nje ya nchi
Vitendanishi: asilimia 100% huagizwa kutoka nje ya nchi

Monday, February 25, 2013

hata mimi, Editha Majura nilikuwepo Mtwara; yaani we acha tu.
Nguli katika tasnia ya habari ndani ya Bongo na 'mji kasoro bahari' nao walikuwepo Mtwara.
Rahel na shost wake huyo, si unamfahamu eh, nao walikuwepo Mtwara.
hao ndiyo John na George Maratu bwana! ndani ya Mtwara

Sharon naye alikuwepo,
Hivi ndivyo Babo alivyopigwa risasi Bagamoyo
Gidalis Babo (18) Mbarbaig, anazungumza akishindwa kuzuia machozi kutengeneza njia mashavuni mwake, anasema mwishoni mwa mwaka jana, yeye na wafugaji wenzake wasiyopungua Kumi, walifatwa na jirani yao kwamba Ng’ombe wake Sita wameibwa.
Jirani yao huyo anayemiliki Ng’ombe 100, inaelezwa kuwa awali alikuta hiyo mifugo yake imewekwa kizuizini na Mzee Chamiwa, kwa kuwakuta wakinywa maji kwenye Bwawa alilotengeneza ndani ya himaya yake.
Babo anasema baada ya mazungumzo (kati yam Chamiwa na jirani yao) waliafikiana kesho yake jirani ya Babo akalipe faini (fedha ingawa haikulezwa kiasi gani) akaruhusiwa kuchukua mifugo yake.
Hatahivyo, Ngiombe walipofikishwa nyumbani na kuhesabiwa ikabainika Sita wamepungu. Ndipo Babo pamoja na wenzake wakakusanyika kuanza kazi ya kusaka Ngiombe waliopotea au ibiwa. Eneo la kwanza waliona vyema waanzie nyumbani kwa Chamiwa.
“Tukiwa nyumbani kwa Mzee Chamiwa hatukuona mtu, tukazunguka zunguka  nyumba ndipo tukaona eneo lililotifuliwa, tulipochimba tukaona vichwa viwili vya Ng’ombe na ngozi zake, kisha tukamuona mtoto wa huyo mzee tukaanza kumuhoji walipo Ng’ombe wengine,” anaeleza Babo.
Anasema wakati wakiendelea kumuhoji, akatokea Mzee Chamiwa akiwa amepakiwa kwenye pikipiki almaarufu bodaboda. Alipoteremka, akawafata huku akiwa na kitu mkononi, inadaiwa Babo hakujua kuwa ilikuwa bunduki, alifikiri ni aina ya fimbo za kujihami.
Anasema aliruka na kushika hiyo fimbo (bunduki) mfugaji mwenzao akawaambia kuwa hiyo ni bunduki, wakimbie lakini kabla hafanya lolote, alishtukia akipigwa na vitu sehemu tofauti za mwili wake na akaanguka, akapoteza fahamu.
Gidufana Gafifem, jamaa yake Babo anasema, wenzao wengi walikimbia baada ya kushuhudia ndugu yao damu zikimtoka kwa wingi.
Anasema aliyempiga risasi Babo alikuwa ndani ya nyumba ya Mzee Chamiwa na kwamba walipoona Babo ameanguka na wenzake wengi wamekimbia, nao wakachomoka kama mishare ndani ya nyumba na kukimbia.
Anasema bunduki aliyokuwanayo Chamiwa walifanikiwa kumnyang’anya. Pamoja na Mzee Chamiwa, silaha hiyo na mabaki ya Ng’ombe wawili waliyoyapata  waliyawasilisha kituo cha polisi Miono.
Hatahivyo, mpaka wakati wakizungumzia tukio hili wilayani Bagamoyo, mtuhumiwa alikuwa uraiani. Wanasema hakuna anayefahamu amepata vipi dhamana kwakuwa hawafahamu kama kuna kesi ilifikishwa mahakamani au la kwakuwa ndugu na jamaa wanahangaika kuuguza ndugu yao Babo.
Usikose awamu ijayo ya taarifa hii, itahusu anachoeleza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi

Friday, February 22, 2013




 Naibu waziri wa afya na ustawi wa jamii, (Mb. Rufiji - CCM) akizungumza kwenye kongamano lililoandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya nchini, (NHIF) ambao umemalizika muda si mrefu mjini Mtwara.
 
 
 
 
 

MFUMO mpya wa utendaji kazi utakaoweza kuunganisha mamlaka zote zinazofanya kazi katika huduma ya afya, unafanyiwa kazi na serikali kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa ujumla, hususan katika upatikanaji dawa zenye ubora katika vituo mbalimbali vya afya.

Naibu waziri wa afya na ustawi wa jamii, ameyazungumza hayo muda dakika chache zilizopita wakati wa kongamano la Nane la wahariri, wanahabari na wadau mbalimbali wa sekta ya afya nchini, ambalo huandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Wanahabari wamefanya tafiti katika wilaya 26 nchini, kuibua yanayojiri juu ya matumizi ya fedha zitokanazo na michango ya mifuko ya NHIF na mfuko wa afya wa jamii, (CHF).

Kila siku ya Jumatano, nitakuwa naleta taarifa za tafiti zilizowasilishwa kwenye kongamano hili, kuanzia wiki ijayo. Usikose na baadaye nakuletea  ‘maneno’ ya mtoto wa kibarbaig wilayani Bagamoyo akieleza alivyopigwa risasi tatu na kupooza.

 

Sunday, February 17, 2013

eti tuisheni kwenye shule za Engilish Medium?
Jamani, hawa walimu wanaofundisha katika shule za msingi za kulipia, a.k.a English Medium, alafu wanatumia mbinu mbalimbali kushawishi wazazi wawalipe fedha ‘vichochoroni’ kwa madai ya kuwafundisha tuisheni watoto wanaakili timamu kweli?
Hivi katika hili wa kulaumiwa ni mwalimu anayedai alipwe ili atumie mbinu za kibindoni za kufundishia kwa mtoto wako au ni mzazi ambaye bila shaka kilichoijaza nafsi yake ni roho ya ubinafsi na uchoyo?
Bila shaka wote wawili mnastahili kulaumiwa, kulaaniwa na hamfai katika jamii kwa maana mnanyong’onyeza elimu nchini.
Mnanyong’onyeza uwezo wa kitaaluma walionao watoto wengine ambao wazazi wao mbali na kumudu kuwasomesha katika shule hizo, hata kama wana pesa za kutoa kununua tuisheni, hawaoni sababu ya kufanya hivyo huku wakilipa milioni kadhaa kila mwaka.

aliyeiro Watanzania, bora awaonee huruma wwakomboe kwa maana hali imefikia ukomo wa ubaya.


GIDALIS Babo (18), bado yupo hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo. Jumatano alipelekwa MOI, ikaamuriwa abaki alipo mpaka Machi 1, mwaka huu atakapopelekwa kutolewa vyuma mkononi.
Taarifa ya alivyojeruhiwa na athari alizopata zimetolewa rasmi:

-         Pingili ya uti wa mgongo imetobolewa kwa risasi, atakuwa kilema milele; hataweza kusimama wala kutembea.
-          Risasi ya mgongoni haikutolewa kwa maelezo kwanga ilivyokaa ingetolewa ingesababisha madhara makubwa zaidi
-          Mkononi pia risasi bado ipo, haijafahamika kama itatolewa au nayo ataendelea kuishi nayo mwilini.

Naandaa taarifa ya Gidalis kuhusu alivyopatwa na mkasa huu, usikose kufuatilia.

 
Kila ninapofikiria huwa nashindwa kuelewa wanaoiba fedha za umma wa watanzania na kuzificha kwenye nchi za wenzao, tena zilizoendelea wana roho ya aina gani; ebu angalia Godoro linalotumiwa na mama, dada, shangazi na wadogo zetu wanapotekeleza jukumu lao la 'kuujaza ulimwengu' kwenye kituo cha afya kilichopo Dodoma, wilayani Maswa.

Kituo kinamilikiwa na serikali, mbali na magodoro kuchakaa hakuna shuka. mgonjwa akiwa na shuka inakuwa nafuu asipokuwa nalo inakuwa kama inavyoonekana.

Friday, February 15, 2013


Serikali yakunjua makucha dhidi ya migogoro baina ya wananchi na wawekezaji
KUTOKA kushoto, Mkurugenzi wa Viwanda vya kuongeza thamani wa Shirika la Maendeleo nchini (NDC), Shannel Mvungi na Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Dk. Anacleti Kashuliza wakikabidhiana mikataba ya ushirikiano.
Leo Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) limetangaza kuunganisha nguvu na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kuwafumbua macho na kuzindua akili za wananchi waone na kutumia fursa zinazokuwepo kwenye maeneo yenye miradi inayoendeshwa na NDC nchini.
Wameanzia kwenye mradi wa uchimbaji wa Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga wilayani Ludewa. Watatoa mafunzo ya kutambua fursa na kuzitumia kukuza uchumi, kuwawezesha kupata mitaji na kuainisha, kuendeleza maeneo huru ya kufanyia biashara.
Kwetu kunamsemo usemao, “Empisi ekanyampila eibale, eti nolwo’otagamba  wakaulila.” Usemi huu unaendana na vurugu za wananchi wakipinga kusafirishwa gesi kutoka huko kupelekwa Dar es Salaam kwani baada ya hayo,  inaashiria serikali imehisi kitu na sasa imeanza kuchukua hatua.



Gidalis Babo (18) Mbarbaig aliyejeruhiwa kwa risasi mwishoni mwa mwaka jana, mkoani Pwani, wilayani Bagamoyo eneo la Miono amepooza. Inadaiwa Daktari wa wodi namba Sita, hataki aendelee kuwapo hospitalini hapo kwa maelezo kuwa amepona.
Ndugu zake wanasema, “Ingawa tunaamini afya yake haijaruhusu aondolewe hospitali, ndugu zetu walio kijijini alivyo huku mtuhumiwa wakipishana naye uraiani, Wabarbaig tunawafahamu wataleta maafa hata kama wanafahamu hawatakuwa salama mikononi mwa polisi,” anaeleza Gidufana Gafifem.
OCD alipopelekewa taarifa zinazoelezwa na ndugu za Babo, akashuhudiwa akimpigia simu DC (Ahmed Kipozi), “Yule kijana aliyejeruhiwa kwa risasi kwenye mgogoro wa wakulima na wafugaji, wakati akitolewa muhimbili hali yake ikawa mbaya ikabidi awekwe hospitali ya wilaya, sasa nasikia wanataka aondoke hospitalini…, tunaomba msaada wako maana hali ya usalama inaweza kuwa shakanai.”
DC alipoulizwa akasema analishughulikia, akasikika akizungumza na mganga wa wilaya (DMO), ikaafikiwa abaki. (taarifa zote hizi zimepatikana Jumamosi, wiki iliyopita.)
Lakini Jumatatu ya wiki hii mmoja wa ndugu wa Babo akapiga simu akisema, Daktari wa wodi amesisitiza mgonjwa tumuondoe akisema,
“Niliwaambia leo mwisho kuwa wodi hii, badala ya kumtoa mnaniletea vyombo vya habari? hata kama uongozi umeniambia abaki, lazima atoke ina maana hawajui kuwa mimi ndiye daktari? Mking’ang’ania namuandikia arudishwe Muhimbili  tuone kama nako mtang’ang’ania.” (sauti ya Daktari akizungumza hayo imerekodiwa)
Je, amebaki wodini?, amehamishiwa muhimbili? Au amefukuzwa? Naendelea kufuatilia; usikose kufungua Double Cleopa kila unapoingia mtanadaoni.