Matukio yanayoendelea kuibuka kila kukicha nchini,
yakihusisha hali ya wananchi kutoridhishwa na matendo au maamuzi kadha wa kadha
yanayofanywa na wanaowaongoza katika nyanja mbalimbali; ni ishara ya kuchoshwa
na mazingira yanayowakabili.
Bila shaka ni ugumu wa maisha. Naamini hivyo
ninapotafakari varangati lililojiri hivi karibuni Liwale, Mtwara.
Kwamba viongozi wa chama cha ushirika cha msingi
Minali, walitaka kuwalipa Sh 200 kwa kilo moja wakulima waliowauzia Korosho kwa
makubaliano ya kuwalipa Sh 1,200 kwa awamu. kwanza Sh 600 alafu Sh 600.
Mmoja wa viongozi hao alikaririwa na vyombo vya
habari akisema makubaliano yalikuwa walipe kiasi hicho cha fedha kwa awamu.
Katika hali ya kawaida, ikiwa wakulima hao waliafiki
makubaliano kiasi cha kutoa mazao yao kwa ushirika huo; ni dhahiri
waliridhishwa na maelezo waliyopewa, hali inayotatiza kwanini wafanye vurugu
kiasi cha kuteketeza mali za viongozi wao.
Mtazamo wangu unaniaminisha kuwa kuna mambo mawili; inawezekana
chama kilieleza kuwa kingelipa Sh 600 kamili kwa awamu ya kwanza lakini Sh 600
ya kumalizia ingelipwa kwa awamu, huku wakulima wafikiri malipo yote
yangefanywa kwa awamu mbili tu.
Au inawezekana viongozi wa ushirika walifikiri
Tanzania ya leo ndiyo ile ya “jana na juzi”, wakataka kuchakachua na wakulima
hawakukubali. Siyo rahisi mtu aliyeafiki kukupa mzigo na kupokea malipo ya
awali, agome kupokea malipo ya mwisho na kufanya vurugu kubwa vile.
Ushauri
Inawezekana nikawa mdogo kiumri,madara na elimu kwa
wanaoongoza umma wa Watanzania lakini nawaasa wasome alama za nyakati,
wabadilike.
Hakuna anayependa kuona viongozi wakidharirishwa kwa mali
zao kuchomwa moto, kutolewa matusi, kuzomewa ilhali wakiwa baba au mama wa
Watanzania wenzetu lakini pia wanatakiwa kutambua kwamba Watanzania wengi
wamekata tamaa.
Hakuna kitu kigumu na cha hatari chini ya jua kama
kuongoza mtu aliyekata tamaa. Utasikia wakitupiana lawama, “mwanasiasa fulani
ndiye amechochea, chama fulani ndicho kinataka nchi isitawalike...,” jamani!
kuna mtu anayeweza kuambiwa ale mavi akayala?
Bila shaka hakuna, hivyo hali inayoendelea nchini
haina budi kuwafikirisha viongozi wenye dhamana; kutambua kuwa muda wa kuongoza
kwa kuahidi maendeleo bila matendo au kutekeleza maendeleo kwa mwendo wa
kinyonga ili matatizo ya watu yaendelee kuwa mtaji wa wanasiasa umetutupa
mkono.Naipenda sana Tanzania, naipenda sana amani na ninatamani kuona mabadiliko kwa mtu mmoja mmoja na hatimaye jamii kwa ujumla. Mungu ibariki Tanzania.